Twaweza.org

Kazi zetu

Twaweza inajitahidi kutoa taarifa zenye manufaa kwa kila mtu, kukuza uwezo wa vyombo huru vya habari na uwezo wa raia kufuatilia upatikanaji wa huduma. Kwa kufuatilia masuala haya kupitia wabia wake, Twaweza inakusudia kujenga kile kinachoitwa “miundohali ya mabadiliko” kwa kujenga juu ya misingi ya kazi za wananchi na kusaidia kuamsha ari ya wananchi ili walete mabadiliko, na kwa kuziendeleza kazi hizo kwa kuziwekea mikondo ya ushirikiano na ubia. Twaweza inayo maeneo matatu ambacho ndicho kiini cha kazi zake: Ukuzaji wa Ubia; Uwazi (Kituo cha Habari), na Mafunzo na Mwasiliano.

Ubia

Ubia katika utekelezaji wa programu ni sehemu muhimu kabisa ya mtazamo wa Twaweza. Kwa kutumia mikondo ya ubunifu kujenga ubia wa kimkakati, Twaweza imedhamiria kusaidia ujenzi wa miundohali itakayowawezesha wananchi kudhihirisha utashi wao – kupata habari, kufuatilia maendeleo, kusema kwa uwazi na kusababisha mabadiliko – na kwa kufanya hivyo wajipatie huduma bora za jamii. Tunashirikiana na wabia katika maeneo ya huduma za maji, elimu na afya, na tunao pia wabia wanaounga mkono juhudi za ujenzi wa utashi wa raia kwa ujumla.

Uwazi

Twaweza imeanzisha kitengo cha Uwazi ambacho kinawapa wabia wa Twaweza, vyombo vya habari na mawakala wakuu wa mabadiliko (wabunge, waandishi wa habari, wakuu wa serikali) taarifa zilizojengwa juu ya msingi wa takwimu, na zinazowasilisha ujumbe ulio wazi na unaoeleweka kirahisi. Soma zaidi kuhusu Uwazi.

Mafunzo na Mawasiliano

Ingawaje Twaweza inahusiana na kutenda, lakini pia inaweka mkazo mkubwa katika mafunzo. Ingawaje kazi zetu zitajengeka juu ya uzoefu uliopatikana toka kote duniani lakini pia tunajaribu mbinu mpya na kufanya majaribio tukitumia mbinu bunifu kadri tunavyoimarisha mahusiano na wabia wetu. Hivyo, tunahitaji ushahidi thabiti wa jinsi kazi zetu zinavyoweza kusababisha mabadiliko ya kudumu katika maisha ya watu. Ubunifu na kujifunza, ufuatiliaji na tathmini, na uwasilishaji wa mafunzo ndizo nguzo imara za mtazamo wa Twaweza.

Twaweza inawahimiza washirika wake kutafakari juu ya utendaji wao ili wajenge utamaduni wa kujifunza, ikiwa ni pamoja na kujikosoa na kujua kwamba hata tunaposhindwa pia ni fursa ya kujifunza kuhusu makosa yaliyofanyika, na kisha kujaribu mbinu tofauti. Twaweza inasisitiza usimamizi-mafunzo (mentoring) wa muda mrefu na inalenga kusaidia kuwapatia wanafunzi wa vyuo vikuu Afrika Mashariki na wale wa kimataifa nafasi miongoni mwa wabia wetu, hususan ili waweze kuandaa nyaraka na kuwasilisha mafunzo yaliyopatikana. Aidha tunafanya kazi kwa karibu pamoja na watathimini huru kutoka nje ili kupata mrejesho wa tafiti zao kuhusu kazi zetu.

"Ni sisi wenyewe!"

Hii ni dhana ambayo ndio msingi wa kuanzishwa Twaweza, kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wanaweza kujiletea maendeleo yao wao wenyewe, badala ya kusubiri kufanyiwa hivyo na serikali, wanasiasa, wafadhili au asasi zisizo za serikali. Kazi yetu katika hili itazinduliwa kwa matangazo kwa umma (matangazo 12 kupitia televisheni na redio) ili kukuza mabadiliko ya kifikra na kujenga utambuzi kwamba huduma bora na uwajibikaji vinawezekana tu iwapo wananchi wenyewe watawajibika na kutenda, ndiyo kusema wakijenga utashi wa kutenda.

 

 

 

zinazotumwa katika RSS

 

Tafsiri