Twaweza.org

Twaweza ni nini

Mabadiliko ya kweli huchukua muda. Si nia yetu  kukurupuka na mambo mepesi mepesi au shughuli ndogondo tu na kisha kuweka tiki ya ufanisi katika mabano. Ndiyo maana Twaweza imejipangia kipindi cha miaka kumi, ikiwa na malengo makuu mawili. Kwanza, tunataka kuimarisha ‘utashi wa wananchi’ kwa maana ya uwezo wa wanaume, wanawake na vijana kupata taarifa zilizo bora na za kuaminika, kwa haraka zaidi na kwa bei nafuu; waweze kufuatilia na kujadili kinachoendelea, waweze kusema kwa uwazi na wachukue hatua kuleta mabadiliko.Hii peke yake ni muhimu, kwa sababu kila mtu anatakiwa ajisikie kwamba anao uwezo au udhibiti juu ya maisha yake. Hili  ni muhimu kwa sababu linashadidia lengo letu la pili, ambalo ni kuwawezesha watu wengi zaidi kujipatia huduma bora za elimu, afya na maji safi. Kwa taarifa mahususi soma zaidi.

Tunafanyaje kazi zetu?

Hatuamini kwamba mabadiliko endelevu yatakuja kwa kuanzisha vijimiradi vidogo vidogo hapa na pale. Na wala hatuamini kwamba watu waliokaa makao makuu (mijini) ndiyo wenye uwezo wa kuleta maendeleo kwa maelfu ya jamii za ukanda huu. Kwa hiyo hatuna mpango wa kuanzisha miradi mingi ya Twaweza. Badala yake tutafanya kazi kupitia mitandao mikubwa na asasi pana ambazo tayari zinawasiliana na wananchi na zinagusa maisha yao, kama vile vyombo vya habari, simu za mkononi, mashirika ya dini na mitandao ya usambazaji bidhaa za biashara za rejareja.Tutasaidia kuimarisha ubia wenye manufaa maradufu, kwa kuinufaisha jamii husika huku kila mbia naye akijisaidia kile ambacho ni ada yake. Na kwa kuwaunganisha wabia ambao kwa kawaida labda wasingeshirikiana –kama vile vyama vya walimu na makanisa au makampuni ya simu za mkononi—tunatajia kubadilisha mazingira ya kiutendaji katika ngazi za msingi. Soma zaidi na uone vigezo vyetu vya ubia.

Kwa nini tunasisitiza kuhusu kujifunza na kufanya tathmini?

Kama ilivyo kwingineko, Afrika Mashariki imetapakaa miradi mingi iliyoanzishwa pengine kwa malengo mazuri tu lakini haikufanikiwa sana au haikudumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo tumenia kuwa makini sana katika kujifunza na kubadilishana uzoefu. Ni sehemu gani zilizifanya vizuri na sehemu gani hazikufanya vizuri, na kwa nini? Ni mambo gani muhimu yanasababisha kushinda au kushindwa, na katika mazingira gani? Wakati wote tutahimiza utamaduni wa kujifunza na kujikosoa, tukihifadhi uzoefu wetu katika nyaraka zilizoandaliwa kwa ubunifu na kwa njia inayoeleweka kirahisi. Aidha tumeiteua asasi huru ili ifanye tathmini ya undani juu ya shughuli za Twaweza katika miaka mitano ya mwanzo, na matokeo ya tathmini hiyo yatatumika kuboresha kazi zetu na kuongeza ujuzi wetu kwa ujumla.

Tuko wapi hadi sasa?

Bado ni mapema sana. Mwaka 2009 tuliweka mkazo katika kufanya utafiti, kuanzisha asasi yenyewe, kuajiri wafanyakazi na kuasisi mifumo. Tuna ari kubwa ya kuzidi kusonga mbele, na tayari tumeanza kufanya kazi na wabia kadhaa na hivi sasa tunaangalia uwezekano wa kufanya kazi na wabia wapya wanaotia moyo.

zinazotumwa katika RSS

 

Tafsiri