Twaweza.org

Utamaduni wa kujifunza

Tunatumia neno ‘kujifunza’ kwa makusudi. Tunaamini kwamba maneno kama ‘mafunzo’ au ‘ujenzi wa uwezo’ ni maneno yanayoashiria elimu ya aina ya ‘kuwekeza katika benki’ yakimaanisha upokeaji wa ujuzi bila ushiriki katika mchakato wa elimu. Kwa kusisitiza ubunifu tunatia mkazo katika kujifunza kulikoratibiwa, kujifunza kwa kutenda, na kutafakari kuhusu kazi zetu pamoja na muktadha wa medani tunamofanyia kazi zetu.Kwa ajili hii tunaendesha mafunzo ya ndani kwa wafanyakazi wetu mara mbili kwa mwezi, klabu ya usomaji makini mara moja kwa mwezi, na kila mwaka tunafanya ziara maalumu ya mafunzo ya nje. Katika mwaka 2010 tutaweka mkazo katika kuandaa makabrasha ya mafunzo kwa ajili ya wabia wetu kwa kuchunguza mahitaji yao, kutoa misaada, kutafakari na kuchangia katika kujifunza kutokana na mafunzo yaliyopatikana.

Ziara za nje

Katika mwaka 2009, ziara yetu ya mafunzo ya nje (iliyofanyika kwa ushirikiano na SNV) iliwahusisha wafanyakazi wote wa Twaweza ambao walikaa kwa muda katika jamii tisa katika kanda ya Ziwa nchini Tanzania. Lengo lilikuwa ni kuwasaidia wafanyakazi waweze kuelewa kwa njia ya moja kwa moja ya hisia zao wenyewe ni jinsi gani miradi ya Twaweza inaweza kuwa, au kutokuwa ya manufaa kwa maisha ya kila siku ya raia wa kawaida wa Tanzania, pamoja na shughuli zao na uzoefu wao. Hivyo tulikusudia kupima uhalisia wa nadharia yetu ya mabadiliko na kuhakikisha kwamba kazi zetu zinajengeka juu ya kile kilichopo tayari na siyo kujaribu kubomoa kilichopo. Katika makundi madogo ya watu wawili wawili au watatu tulikwenda kuishi katika vijijini vinane na sehemu moja ya mjini katika kanda ya Ziwa. Kwa muda wa siku tatu tuliishi na familia za wenyeji wetu na kuwafuatilia katika shughuli zao za kila siku na kufuatilia maeneo mbali mbali ya mazingira wanamoishi, na kisha tukawa na siku mbili za kutafakari kuhusu mambo tuliyojifunza. Bonyeza hapa kuona taarifa ya power point

Wakufunzi wakazi wa Twaweza

Wakufunzi wakazi ni sehemu muhimu sana ya kazi za Twaweza, na tunakaribisha maombi ya wanafunzi kutoka Afrika Mashariki na duniani kote. Mnamo mwaka 2009 tulikuwa na wakufunzi saba waliofanya kazi nasi, watano kutoka Tanzania, mmoja kutoka Marekani na mmoja toka Norway. Wakufunzi wameisaidia Twaweza katika ufuatiliaji na tathmini, utawala na mawasiliano, kutenegeneza ramani na ufuatiliaji wa raia kwa kutumia simu za mkononi. Mwaka wa 2010 wakufunzi watapelekwa kufanya kazi miongoni mwa asasi za wabia wetu, ambako watafanya kazi za utafiti na kuandaa nyaraka na kuchangia uzoefu kuhusu miundo ya upatikanaji wa habari, vyombo vya habari, teknolojia za mawasiliano na kuzihusianisha na utashi wa raia. Aidha tutaendelea kuwa na wakufunzi hawa katika ofisi za Twaweza wakitusaidia katika maeneo makuu ya shughuli zetu: ubia, kujifunza na mawasiliano,kituo cha Uwazi na utawala.

Tafadhali wasiliana nasi iwapo unapenda kuwa mkufunzi mkazi. Ili kupata fomu ya maombi bonyeza hapa, ijaze, kisha tupelekee kwa anwani (barua pepe): interns@twaweza.org. Tafadhali kumbuka kwamba tunahitaji wasifu wako (CV) , namna ya kuwasiliana nawe, wadhamini wawili, kazi mbili ulizoandika na eneo la kazi unalopendelea.

zinazotumwa katika RSS

 

Tafsiri