Twaweza.org

Je, watoto wetu wanajifunza?

Baadhi ya watoto wa darasa la 7 hawawezi kufanya majaribio ya darasa la 2. Wanafunzi wanne kati ya kumi (44%) hawawezi kusoma hadithi ya Kingereza ya kiwango cha darasa la pili, wawili kati ya kumi (16%) hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili, na wawili kati ya kumi (23%) hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la pili.

Watoto kutoka familia zenye uwezo, au wanaoishi mijini wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata stadi za msingi za kusoma na kufanya hesabu.  kuliko wenzao wanaotoka familia maskini au wanaoishi vijijini. Pamoja na mafanikio yanayoonekana kwenye ongezeko la unadikishaji wa wanafunzi, Tanzania bado haijatimiza dhamira yake iliyojiwekea chini ya malengo ya Elimu Bure kwa Wote. Hususani, bado hakuna usawa kwenye vifaa vya shule na mazingira, uandikishaji na matokeo ya kujifunza.

Matokeo haya yametolewa na Uwezo Tanzania kwenye ripoti yao iitwayo Je, Watoto Wetu Wanajifunza? Hali ya elimu nchini Tanzania mwaka 2015 (Kiingereza - soma muhtasari kwa Kiswahili). Ripoti hii inatokana na takwimu za tathmini zilizokusanywa na Uwezo iliyopo Twaweza. Tathmini hii inaongozwa na wananchi katika kupima matokeo ya kujifunza nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Katika awamu ya tano ya ukusanyaji wa takwimu uliofanywa na Uwezo Tanzania mwaka 2014, jumla ya watoto 32,694 walipimwa kutoka kaya 16,013. Takwimu pia zilikusanywa kutoka shule za msingi 1,309.

Matokeo ya masomo yote matatu yaliyopimwa na Tathmini ya Uwezo ya Mwaka ya Kujifunza yameendelea kubaki chini. Katika darasa la 3;

  • 54% ya wanafunzi wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili
  • 19% tu ya wanafunzi wanaweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili
  • 35% tu ya wanafunzi wanaweza kufanya hesabu za darasa la pili

Katika kipindi cha miaka mitano ya tathmini za Uwezo, kumekuwa na mabadiliko finyu kwenye matokeo ya kujifunza. Hatahivyo, viwango vya ufaulu vya Kiswahili vinaonesha matokeo chanya. Kwa mfano, kati ya 2012 na 2014, idadi ya wanafunzi wa darasa la 3 ambao wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la 2 imeongezeka kutoka 26% mpaka 54%. Hata hivyo, matokeo haya bado yapo chini ya kiwango kilichopangwa na mtaala.

Matokeo ya Uwezo yanaonyesha kuwa hakuna usawa katika mzunguko wote wa elimu kuanzia upatikanaji wa elimu hadi vifaa na matokeo ya kujifunza.

Kitaifa, 65% ya watoto hawajaandikishwa katika shule za awali na kati yao 84% wanaishi maeneo ya vijijini.

Kati ya watoto walioandikishwa shule za awali, 62% wanatoka kwenye kaya zenye uwezo, huku 23% pekee wakitoka kaya masikini.

Kwa ujumla, kati ya 19.2% ya watoto ambao hawakuwa shuleni; zaidi ya nusu walitoka kaya masikini.

Vilevile, kuna tofauti kubwa  kati ya mkoa mmoja hadi mwingine husuani katika idadi ya watoto wenye umri wa miaka 7-16 ambao hawapo shuleni. – 8% ya watoto wanaotoka mkoa wa Dar es salaam wenye umri wa miaka 7-16 hawapo  shuleni ukilinganisha na 35% wa mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wa mazingira ya shule, ipo pia tofauti kubwa kati ya mkoa mmoja hadi mwingine:

Utoro wa walimu ni: 58% mkoa wa Singida ukilinganisha na 17% mkoani Ruvuma na Manyara.

Uwiano wa wanafunzi kwa mwalimu ni: wanafunzi 126 kwa mwalimu mmoja katika mkoa wa Mara na wanafunzi 56 kwa mwalimu mmoja katika mkoa wa Pwani.

Uwiano wa wanafunzi kwa kitabu ni: wanafunzi 26 kwa kitabumkoa wa Tabora na wanafunzi 3 kwa kitabu mkoani Mtwara, Kilimanjaro, Katavi, Ruvuma na Njombe.

Uwiano wa wanafunzi kwa choo: mkoa wa Simiyu, wasichana 261 hutumia tundu moja la choo  na wavulana 259 hutumia tundu moja wakati mkoani Njombe tundu moja la choo hutumiwa na wasichana 52 na vilevile wavulana 59 hutumia tundu moja la choo.

Kwa upande wa matokeo ya kujifunza, watoto wa mijini wanafanya vizuri kuliko wenzao wa vijijini.

Vilevile, matokeo yanatofautiana kati ya mkoa mmoja na mwingine: 81% ya watoto wanaotoka mkoa wa Dar es salaam wenye miaka 9 hadi 13 walifaulu jaribio la Kiswahili ukilinganisha na 28% wa mikoa ya Mara na Rukwa. Takriban watoto watano kati ya kumi (55%) wenye miaka 9 hadi 13 kutoka mkoa wa Arusha walifaulu jaribio la Kingereza wakati ni 6% tu ya wale wa mkoani Rukwa waliofaulu. Kwa upande wa Hisabati, 67% ya watoto mkoani Arusha wanaweza kufanya hesabu za kuzidisha, lakini mkoani wa Rukwa ni 20% pekee ndio wanaoweza.

Hali ya uchumi pia inaonekana kuchangia matokeo ya kujifunza. Karibu nusu ya watoto (44%) kutoka kaya zenye uwezo walifaulu jaribio la Kiswahili ukilinganisha na 15% tu kutoka kaya duni.

Endelea kusoma:

Authors: Richard Shukia

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri