Twaweza.org

Ushirikiano wa Serikali Zilizo Wazi Waanza Kazi Afrika Mashariki

Ushirikiano wa Serikali Zilizo Wazi (Open Government Partnership-OGP) ulizinduliwa rasmi jijini New York, 20 Septemba 2011 na Rais Barack Obama. Wawakilishi toka nchi 40 walihudhuria uzinduzi wa OGP, wakiwamo Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Zuma wa Afrika Kusini, na mawaziri toka Kenya. Kutoka Afrika ni nchi sita tu zilikidhi vigezo vya msingi kujiunga na ushirikiano huu, kati ya hizo, tano zilijiunga na sasa zinaandaa mikakatiya kitaifa ya utekelezaji wa kanuni za Ushirikiano huo.

Kiongozi wa Twaweza,  Rakesh Rajani, aliongea kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Asasi Zisizo za Kiserikali katika nafasi yake kama mjumbe wa Kamati Ongozi ya OGP. Katika hotuba kuhitimisha hafla hiyo Rais Obama alisisitiza mchango wa uwajibikaji unaoendeshwa na raia na akarejea kipekee hotuba ya Rakesh Rajani.

Ushirikiano wa Serikali Zilizo Wazi ni jitihada mpya ya kimataifa yenye lengo la kuibua utashi madhubuti kwa serikali kuchochea uwazi, kuwawezesha raia, kupambana na rushwa na kutumia technolojia mpya kuboresha utendaji serikalini.

Ili kujiunga na OGP, nchi washiriki lazima zikubali kuanza kutekeleza Azimio la Serikali Wazi. Nchi wanachama zinatakiwa kutekeleza mpango kazi wa utekelezaji wa kanuni za OGP unaondaliwa kwa kushirikisha umma; na pia nchi wanachama zapaswa kuruhusu uchunguzi huru wa hatua wanazopiga.

Uzinduzi wa OGP ulifuatiliwa kwa makini na vyombo vya habari duniani kote. Gazeti la East African liliripoti na kuchapa makala mbili kuhusu OGP :Serikali zinazoshirikisha raia ndio zitafanikiwa, na Marekani yaipongeza Kenya na Tanzania, na kurejea kuchapa hotuba ya Rajani  kama makala huru.

Rais Kikwete ameongelea OGP na kushukuru mchango wa Twaweza, hasa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Septemba 2011. Habari Leo, liliandika kuhusu hotuba hiyo na kuzungumzia OGP na Twaweza.

Kufuatia hayo, Twaweza, kwa kuitikia wito wa Rais Kikwete, imetoa maelezo kuhusu Ushirikiano wa Serikali Zilizo Wazi kwa nyakati tatu tofauti kwa maofisa wa juu wa Serikali Ikulu, kwa Makatibu Wakuu na kwa Baraza la Mawaziri. Unaweza kunyonya taarifa za maelezo hayo hapo chini. Katika mikutano hii Rais Kikwete amesisitiza hitaji la kuwa wazi kwa raia katika mambo yanayowagusa, mathalani huduma za msingi na mambo ya fedha za umma. Rais amemteua Waziri wa Utawala Bora, Mathias Chikawe, kuongoza mchakato huo kwa niaba ya Serikali. Twaweza itasaidiana na Serikali kupata maoni ya umma na kuandaa mpango wa awali wa utekelezaji wa kanuni za Serikali Wazi nchini Tanzania.

Kilicho mbioni sasa ni kutekeleza mashauriano ya umma na kuandaa mpango kazi wa awali kabla ya Mkutano wa Mawaziri toka Serikali wanachama wa OGP huko Brazil Desemba 7. Twaweza imejitolea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kukamilisha andiko hilo.

Endelea kusoma: governance

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri